UHAKIKI WA DIWANI YA WASAKATONGE
Mwandishi: Muhammed S. Khatib
Mchapishaji: Oxford University Press
Mwaka: 2003
UTANGULIZI
Uhakiki umefanyika
katika diwani ya Wasakatonge.Diwani hii ina jumla ya mashairi sitini na moja
(61). Lakini kwa nia ya kurahisisha uelewa mashairi machache tu yameteuliwa kutoka
katika diwani hii na kufanyiwa uchambuzi wa kina. Haufungwi na uteuzi wa mashairi
haya tu, unaweza kwenda mbali zaidi na ukajifunza mashairi mengine zaidi ya
haya kutoka katika diwani hii. Hilo pia litakusaidia kupanua uelewa wako juu ya
tasnia ya ushairi na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufaulu somo la Kiswahili
katika mitihani ya Kiswahili hapo shuleni kwako na pia katika mtihani wako wa
taifa wa kidato cha nne.
1. Wasodhambi
1.
Wasodhambi!
Wako wapi? Ni wangapi?
Nchi zipi? Chao kipi?
Haki ipi? Nakuwa vipi?
Nauona,
Unafiki.
2.
Wavilemba!
Wavilemba, na majoho,tasibihi,
Wajigamba,safi roho, ni kebehi,
Wanotenda,
Unafiki.
3.
Warozari!
Misalaba, na majuba, na hotuba,
Nyingi toba, zenye hiba, na haiba,
Mambo yao,
Unafiki.
Fani
Mtindo
Shairi la wasodhambi ni shairi la kisasa. Mpangilio wake
unaonesha kuwa shairi hii ni huru, halifungwi na kanuni za kimapokeo.
Muundo
Muundo katika ushairi huzingatia idadi y mistari katika
shairi. Idadi ya mistari ni mitano (5) hivyo muundo wake ni takhmisa.
Taswira
Mshairi ametumia taswira zifuatazo katika shairi hili ili
kujenga picha kwa wasomaji:
Wasodhambi
– muunganiko wa maneno mawili: wasio na dhambi.
Wavilemba
– watu wenye maadili
Majoho
– watu wasomi
Warozari
– wakristu safi
Misaraba
– wakristu safi
Majuba
– waislamu safi
Tasibihi
– waislamu safi
Hotuba
– wanasiasa/ wasomi
Dhamira
Shairi hili linadhamira kuu moja:
Unafiki
: ni kitendo cha …mshairi anaonesha kuwa baadhi watu
wanaoonekana watakatifu mbele za macho ya jamii huwa ni wanafiki kwa kuwa
wanafanua dhambi kama watu wengine. Kwa mfano katika ubeti wa pili mshairi
anasema:
“…Wajigamba,safi roho, ni kebehi,
Wanotenda,
Unafiki.”
Mshairi anatumia taswira kama; waviremba, majoho, tasibihi
na majuba ili kuwasilisha watu wema. Lakini katika uhalisia watu hawa
wanamatendo ya dhambi kama watu wengine.
2. Wasakatonge
1.
Wasakatonge
na juakali
Wabeba zege ya maroshani,
Ni msukuma mkokoteni,
Pia makuli bandarini,
Ni wachimbaji wa migodini,
Lakini
maisha yao chini.
2.
Juakali
na wasakatonge
Wao ni manamba mashambani,
Ni wachapa kazi viwandani,
Mayaya
na madobi wa nyumbani,
Ni matopasi wa majaani,
Lakini
bado ni masikini.
3.
Wasakaatonge
na juakali
Wao huweka serikalini,
Wanasiasa madarakani,
Dola ikawa mikononi,
Wachaguliwa wa ikuluni,
Lakini
wachaguaji duni.
4.
Juakali
na wasakatonge
Wao ni wengi ulimwenguni,
Tabaka lisilo ahueni,
Sikuzote wako matesoni,
Ziada ya pato hawaoni,
Lakini
watakomboka lini?
Fani
Mtindo
Shairi la wasakatonge ni shairi la kisasa. Mpangilio wake
unaonesha kuwa shairi hili ni huru, halifungamani na kanuni za kimapokeo.
Muundo
Idadi ya mistari katika shairi hili ni mistari sita (6).
Hivyo muundo wake ni Tarsidisa.
Matumizi
ya Tamathali za Semi
Taswira
Mshairi ametumia taswira mbili kujenga picha kwa wasomaji:
Juakali - hali
ngumu ya maisha wanayoishi watu wa tababka la chini.
Wasakatonge - watu wenye hali ngumu kimaisha,hasa kupata
chakula cha siku husika. Wao hutafuta pesa ya kujikimu kwa siku chache na
isiyoweza kuweka akiba. Hivyo kila siku wao husaka tonge na si ziada.
Mbinu
nyingine za kisanaa
Dhamira
Umasikini:
ni hali ya kushindwa kukidhi mahitaji muhimu ya maisha. Wasakatonge wanaoneshwa
kuwa ni watu masikini. Mshairi anasema:
“…Ni matopasi wa majaani,
Lakini
bado ni masikini…”
Utabaka:
Kundi la watu katika jamii linalojitofautisha na kundi jingine kwa misingi ya
kiuchumi na kielimu. mshairi anaonesha kwamba katika jamii yetu kuna utabaka.
Anaenda mbali zaidi na kuonesha kwamba wasakatonge ni watu wa tabaka la chini.
Anaposema:
“…Wao ni wengi ulimwenguni,
Tabaka lisilo ahueni…”
Unyonyaji:
ni hali au tabia ya mtu au kikundi kupokea mapato makubwa bila ya kufanya kazi
au kwa kufanya kazi kidogo. Mshairi
katika ubeti wa kwanza anonesha kuwa watu wa tabaka la chini hufanya kazi nzio
na za nguvu kunufaisha wenye pesa lakini wao siku zote hubaki masikini.
“…ni wachimbaji wa migodini,
Lakini maisha yao chini…”
3.
Hatuna
kauli
1. Hatuna
sisi kauli,
Ni kwa yetu sisi maduhuli,
Si
umma si serikali.
2. Mavuno
yetu shambani,
Madini ya aridhini,
Ulaya
bei ni duni.
3. Vitu
vyao viwandani,
Madawa pia mashini,
Bei
zake za thamani.
4. Maagizo
tunapewa,
Mipango tunapangiwa,
Na
amri tunatolewa.
5. Sera
zote sio zetu,
Zimeletwa huku kwetu
Hazina
faida katu.
6. Twapewa
yake mitaji
Tuwe wasimamiaji
Pia
watekelezaji
7. Tunatumia
nguvu zetu
Bila kupata kitu
Chenye
na faida kwetu.
8. Hakika
ni uonevu,
Kwa kujifanya werevu
Wenye
mbinu za mabavu.
Fani
Mtindo
shairi la hatuna kauli ni shairi la kisasa, mpangilio wake
haufungwi na kaida za kimapokeo.
Muundo: shairi hili lina,uumdo wa tathilitha; idadi ya
mistari ni mitatu (3).
Taswira
Taswira zilizotumika
katika shairi hili hasa ni jina la shairi; kimsingi jina hili linasimamia dhana
kwamba nchi za kiafrika bado ziko chini ya ukoloni.
Dhamira
Unyonyaji:
ni hali au tabia ya nchi au kikundi cha watu kupokea mapato makubwa bila ya
kufanya kazi au kwa kufanya kazi kidogo. Mshairi anaonesha dhamira hii katika
ubeti wa pili anapojadili juu ya bei za mazao na madini yanayotoka katika nchi
zetu katika soko la dunia. Anasema:
“Mavuno yetu shambani,
Madini ya aridhini,
Ulaya bei ni duni”
Ukandamizaji:
ni hali au namna ambayo kundi Fulani la watu hunyima haki wananchi wengine
katika mambo ya kisiasa na uchumi. Dhana ya ukandamizaji imejadiliwa katika
shairi hili, mshairi anafafanua namna bidhaa kutoka nchi za magharibi
zinavyouzwa kwa bei ghali ukilinganisha na bidhaa kutokakwetu Africa. Katika
ubati wa tatu, mshairi anasema:
“Vitu vyao viwandani,
Madawa pia mashini,
Bei zake za thamani”
Ukoloni
mamboleo: ni namna ya utawala wa chi za kibepari ya kuathiri na
kuamua juu ya uchumi na siasa ya nchi zinazoendelea kwa maslahi yao. Mshairi
anagusia suala hili anapojadilijuu ya mataifa ya ulaya na jinsi yanavyozipangia
nchi za kiafrika sera na utekelezaji wake. Katika ubeti wa nne mshairi anasema:
“Maagizo tunapewa,
Mipango tunapangiwa,
Na amri tunatolewa”
4.
Mwanamke
1. Namwona
yu shambani,
Na jembe mikononi,
Analima
Mwanamama,
Mavuno si yake,
Ni ya mume wake.
2. Namwona
viwandani,
Pia maofisini,
Yu kazini,
Hamkani,
Anabaguliwa,
Na anonewa.
3. Namwona
yu nyumbani,
Mpishi wa jikoni,
Yaya yeye,
Dobi yeye,
Hakuna malipo
Likizo haipo.
4. Namwona
kitandani,
Yu uchi maungoni,
Ni mrembo,
Kama chombo,
Chenye ushawishi,
Mzima utashi.
5. Namwona
mkekani,
Yuwamo uzazini,
Apumua
Augua,
Kilio cha kite,
Cha mpiga pute.
6. Kwa
nini mwanamke,
Ni yeye peke yake,
Anyimwaye,
Heshimaye,
Haki anakosa,
Kwa kweli ni kosa.
Fani
Mtindo
Shairi la Mwanamke ni shairi la kisasa, mpangilio wake na
idadi ya mistari havifungwi na kaida za kimapokeo.
Muundo
Idadi ya mistari katika shairi hili ni mistari sita (6).
Hivyo muundo wake ni Tarsidisa.
Dhamira
Kimsingi shairi hili linamuangaza mwanamke wa kiafrika na
kujadili changamoto zinazomkabili katika maisha ya kila siku.
Dhamira kuu ni nafasi ya mwanamke katika jamii. Mshairi
anamfafanua mwanamke wa kiafrika kama :
Ø Mchapakazi:
mwanamke wa kiafrika hujituma katika kazi za shamba na kazi nyingine lakini
kipato hubaki kwa mumewe. Katika ubeti wa kwanza mshairi anasema:
Namwona yu shambani,
Na jembe mikononi,
Analima
Mwanamama,
Mavuno si yake,
Ni ya mume wake
Ø Kiumbe anayebaguliwa:
Dhana hii inajitokeza hasa kwa wanawake waliopata nafasi ya kusoma na kuelimika.
Baadhi ya wanajaimii huwabagua na kuwatenga wanawake walioelimika kwa kisingizio
cha maringo. Mshairi analiona hili, katika ubeti wa pili (2) analifafanua na
kuliweka bayana. Anasema:
Namwona viwandani,
Pia maofisini,
Yu kazini,
Hamkani,
Anabaguliwa,
Na anonewa.
Ø Mama wa Nyumbani:
Mshairi anamuonesha mwanamke wa kiafrika kama mama wa nyumbani, ambaye anafanya
kazi nyingi bila mapumziko. Hali hii inasababishwa na mfumo dume katika jamii
yetu. Mfumo huu unamkandamiza mwanamke na kumfanya kuwa mtu anayepaswa kufanya
kazi za nyumbani pekee pasi kupata msaada kutoka kwa mwanaume. Katika ubeti wa
tatu msshairi anasema:
Namwona yu nyumbani,
Mpishi wa jikoni,
Yaya yeye,
Dobi yeye,
Hakuna malipo
Likizo haipo.
Ø Chombo cha Starehe:
Dhana hii imejengeka miongoni mwa wanajamii hususan wanaume. Wanaume wengi
wanaamini kwamba mwanamke yupo kwa ajili ya kuwafurahisha wao kimwili. Mshairi analigusia
suala hili na kuweka wazi namna mwanamke wa kiafrika anavyochukuliwa kama
chombo cha starehe. Katika ubeti wanne anasema:
Namwona kitandani,
Yu uchi maungoni,
Ni mrembo,
Kama chombo,
Chenye ushawishi,
Mzima utashi
Ø Kiumbe Duni:
Mwanamke wa kiafrika amekuwa akinyimwa haki zake za msingi na amekua akikosa
namna kujitetea. Katika kulifichua na kuliweka wazi suala hili mshairi katika
ubeti wa sita anasema:
Kwa nini mwanamke,
Ni yeye peke yake,
Anyimwaye,
Heshimaye,
Haki anakosa,
Kwa kweli ni kosa.